Saturday, November 26, 2016

HAJI MANARA MTOTO WA NGULI WA SOKA NCHINI ALIEBANIWA KULISAKATA SOKA

Wachezaji wengi wa zamani wamerithiwa na watoto wao vipaji vya kucheza soka na watoto hao wanatamba kwenye medani ya mchezo huo kama ilivyokuwa kwa wazazi wao na hapa ndipo usemi wa ‘maji hufuata mkondo’ unapotimia.

Ma-star wanaotamba kwasasa ambao wazazi wao walishawahi kucheza soka la kiwango cha juu ni pamoja na Himid Mao wa Azam FC huyu ni kiungo wa kutumainiwa kwenye klabu yake na timu ya taifa, babayake mzazi mzee Mao Mkami enzi zake pia aliwahi kutamba kwenye soka la Tanzania. Mrisho Ngassa aliekuwa akiyecheza soka la kulipwa huko nchini Afrika ya Kusini na sasa yupo Uarabuni baba yake Halfan Ngassa alikuwa nyota wa soka nchini miaka ya nyuma.

Swali linakuja kwa Haji Manara mtoto wa mchezaji wa zamani aliyewahi kutikisa kwenye soka la Bongo, Sunday Manara ‘Computer’ yeye imekuaje hajasikika kwenye soka la hatua ya ligi yoyote, je soka limempitia pembeni?

Haji Manara ambaye ni Afisa Habari wa Klabu ya Simba alilijibu swali hilo kwa kusema,  “Baba yangu hakutaka nicheze mpira, baba yangu katika hilo alinibania kabisa. Kwasababu kwanza alinihimiza kwenye mambo ya shule. Kuna wakati nilikuwa nasoma Mzumbe, nilikuwa naupiga mwingi sana nikachaguliwa combaini ya UMISETA Kanda ya Mashariki. Kambi ilikuwa Kilosa kocha wetu alikuwa Maulidi Dilunga”, amesema Manara.

“Baba alivyogundua vile, akaja akanitoa haraka. Kwahiyo suala la mimi kwanini sichezi mpira ni kutokana na mzee mwenyewe. Lakini simlaumu kwa hilo kwasababu alikua na nia thabiti ya mimi kufanikiwa kielimu. Pengine ningekuwa nacheza mpira leo nisingekuwa nafanya majukumu ninayoyafanya sasa. Lakini yote kwa yote yupo mdogowetu mwingine wa mwisho anaitwa Manara, huyo ndiyo copy ya mzee Manara atakuja kuwa sawasawa”.

Haji Manara pia ni mchambuzi wa masuala ya soka ambapo ameshawahi kufanya uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya television nchini, na sasa anakuja na uwanja wake huu unaokwenda kwa http://hajimanara.blogspot.com ambapo hapa atakuwa anakuletea mambo mbalimbali yahusuyo soka zikiwemi makala za kuvutia. anakukaribisha sana wewe mdau wa michezo katika Uwanja wake huu.